back page

SEHEMU YA PILI

next page

 

Kuwafikishia watu wote ujumbe

Hadithi hii tukufu ilitoka kinywani kitukufu cha Mtume (s.a.w.a) katika sehemu nyingi tofauti tofauti, kiasi cha kudhihirisha kuwa lengo lake likikuwa kuu-fikisha ujumbe huu kwa waislamu wote ili kutimiza hoja kwa umma wa kiislamu.

(a) Siku ya arafa: Miongoni mwa sehemu hizi ni siku ya arafa kama ilivyo katika Sunanut Tirmidhi, kwa Sanadi ya Jaabir ibnu Abdillah, ya kwamba alisema.

(رأيت رسول الله(ص) في حجته يوم عرفة وهو على ناقته القصواء يخطب فسمعته يقول: ((يا أيها الناس اني تركت فيكم ما ان اخذتم به لن تضلوا: كتاب الله، وعترتي اهل رواية)).

“Nimliwona Mtume Mtukufu (s.a.w.a) katika hijja yake siku ya arafa, huku akiwa juu ya ngamia wake (aitwaye) qaswa akihutubu, nikamsikia akisema. “Enyi watu, hakika mimi ninaacha kati yenu ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea kamwe, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu (ambao ndio) wapokezi wa hadithi zangu)”([1])

(b) Huko mina: Miongoni mwazo ni Mina, kama ilivyo katika kitabu cha Ghaibatun Nu’umani, kwa sanadi ya Hariz ibnu Abdillah kutoka kwa Abu Abdillah Ja’afar ibnu Muhammad (a.s) kutoka kwa babu yake (a.s.) kutoka kwa Ali(a.s.), ya kwamba alisema,

((خطب رسول الله (ص) في مسجد خيف – قال ((اني فرطكم وانكم واردون علي الحوض حوضاً عرضه ما بين بصرى الى صنعاء فيه قدحان عدد نجوم السماء، الا واني مخلف فيكم الثقلين: الثقل الاكبر والثقل الاصغر الثقل الاكبر القرآن والثقل الاصغر عترتي أهل بيتي هما حبل ممدود بينكم وبين الله جل وعز ما ان تمسكتم به لن تضلوا سبب منه بيد الله وسبب بأيديكم)).

“Mtume Mtukufu(s.a.w.a) alihotubia katika masjid-ul khiif – (nayo ni khutba mashuhuri katika hijja yake ya mwisho) na kusema “Hakika mimi ninawatangu-lieni, nanyi mtanikuta kwenye hodhi. Hodhi ambayo upana wake ni (mfano wa umbali ulioko) baina ya Basra na Sana. (Kwenye hodhi hii) kuna vyombo vya kunywea (maji ya kauthar) kwa idadi ya nyota za binguni. Basi jueni kwamba, Mimi ninaacha kati yenu viwili vizito; kizito kikubwa na kizito kidogo; kizito kidogo ni kizazi changu (ambao ni) ahlu baiti wangu. Hivi viwili ni kamba iliyonyooshwa baina yenu na baina ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka na Mwenye Nguvu, ambavyo mkishikamana navyo hamwezi kupotea kamwe. Upande mmoja uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na upande mwingine uko mikononi mwenu”.

(c) Huko Ghadir Khum: Miongoni mwa sehemu hizi ni Ghadir khum. Kama ilivyo katika Musta-drakul Haakim na katika vitabu vinginevyo, kutoka kwa Zaid ibnu Arqam, alisema “Mtume Mtukufu alipo kuwa akirejea kutoka hijja yake ya mwisho na kufikia (sehemu iitwayo) Ghadir aliamrisha kuwa miti mikubwa ikatwe, (waislamu wakafanya kama alivyo-sema) na kuitumia katika kuitengeza mimbar, kisha akasema;

((كأني قد دعيت فأجبت اني تارك فيكم الثقلين احدهما اكبر من الآخر كتاب الله وعترتي فانظروا كيف تخلفوني فيهما فانهما لن يتفرقا حتى يردا علي الحوض)).

“Naona kuwa nimeitwa (na Mola) nami nikajibu. Mimi ninaacha kati yenu viwili vizito, kimoja ni kikubwa zaidi kuliko kingine (nacho ni) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu. Basi angalieni vile mtakavyo vitendea baada yangu kwani havitatengana kamwe mpaka vitakaponijia katika hodhi (ya kauthar)”. Kisha akaseme,

((ان الله عزوجل مولاي وانا مولى كل مؤمن))

“Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye  Nguvu na aliyetukuka ni Bwana wangu nami ni bwana wa kila Muumini” kisha akachukua mkono wa Ali (a.s) na kusema,

((من كنت مولاه فهذا وليه)).

“Ambaye mimi na bwana wake basi huyu ni bwana wake”.([2])

Muslim katika Sahihu Muslim([3]) Attabrani katika Almu’ujamul Kabir([4]) na wengineo([5]) wameinukuu hii hadithi.

(d) Huko Madina: Miongoni mwa sehemu hizo ni Mji Mtukufu wa Madina, pale alipokuwa akirejea kutoka safarini, kama alivyopokea ibnu Almaghazili Ash-shafii katika Kitabu chake cha manaqib kutoka kwa Alhaakim, kutoka kwa Ibnu Abbas, ya kwamba alisemu, “Mtume alirudi kutoka (mojawapo ya) safari zake huku rangi (ya uso wake) ikiwa imebadilika. Alitoa hotuba yenye ufasaha wa hali ya juu huku akilia, kisha akasema,

((ايها الناس قد خلفت فيكم الثقلين كتاب الله وعترتي))

“Enyi watu hakika nimacha vizizo viwili kati yenu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu”.

(d) Katika hotuka yake ya mwisho: Na miongoni mwazo ni hotuba yake ya mwisho (wa uhai wake) kama ilivyo katika Yanabiul Mawaddah kutoka kwa Alhamwini, ya kwamba Ali (a.s) alisema”,

((وفي آخر خطبة النبي(ص) يوم قبضه الله عزوجل: اني تركت فيكم امرين لن تضلوا بعدي ان تمسكتم بهما: كتاب الله عزوجل وعترتي اهل بيتي فان اللطيف الخبير قد عهد الي انهما لن يفترقا حتى يردا علي الحوض كهاتين ـ وجمع مُسّبحتيه ـ ولا اقول كهاتين ـ وجمع مسبّحته والوسطى ـ فتمسكوا بهما ولا تقدموهم فتضلوا)).

“Na katika hotuba ya Mtume Mtukufu (s.a.w.a) ya mwisho katika siku ile aliyoaga dunia na kurudi kwa Mola wake(alisema); “Hakika mimi ninayaacha mambo mawili (kati yenu) mkishikamana nayo hamtapotea kamwe baada yangu; Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na aliyetukuka, na kizazi changu (ambao ni) Ahlubaiti wangu; kwani Mjuzi wa yaliyo-fichika na yaliyodhahiri amenijulisha ya kwamba mambo (haya mawili) hayatotengana kamwe mpaka yatakaponijia katika hodhi (ya kauthar) kama hivi viwili – (akavishikanisha vidole vyake viwili vya shahada) na wala sisemi kama hivi viwili – (akaki shikanisha kidole chake cha shahada na kidole cha kati) – basi shikamaneni nayo (mawili) na wala msi-watangulie (Ahlu baiti) msije mkapotea”.([6])

Vile vile imepokewa mfano wake katika Gha-ibatun Nu’umani([7]) na katika Arjahul Matalibi.([8])

Katika uganjwa wake (s.a.w.a): Na miongoni mwazo ni katika ungojwa wake ambao alifariki nao, kama ilivyo katika Yana biul Mawaddah Mwandishi wake amesema kuwa “Ibnu Uqba ameinukuu kutoka kwa njia ya upokezi ya urwa ibnu Kharijah kutoka kwa Fatima Azzahrah (a.s) ya kwamba alisema:

((سمعت ابي (ص) في مرضه الذي قبض فيه يقول وقد امتلأت الحجرة من اصحابه: ايها الناس يوشك ان اقبض قبضاً سريعاً وقد قدمت اليكم القول معذرة اليكم، الا واني مخلف فيكم كتاب ربي عزوجل وعترتي اهل بيتي ثم اخذ بيد عليّ فقال هذا علي مع القرآن والقرآن مع علي لا يفترقان حتى يردا علي الحوض فاسألكم ما تخلّفون فيهما)).

“Nilimsikia baba yangu (mpendwa) (s.a.w.a) katika ugonjwa wake aliofariki nao akisema, huku chumba chake kimejaa maswahaba wake, “Enyi watu, kifo changu kimekaribia sana, nami nime watangulizieni kauli, ili msiwe na udhuru (wa kutoa baada yake). Basi jueni kuwa nakiacha kati yenu Kitabu cha Mwen-yezi Mungu Mwenye Nguvu na Aliyetukuka, pamoja na kizazi changu (ambao ni) Ahlubaiti wangu”. Kisha akaushika mkono wa Ali (a.s) na kusema, “Huyu Ali yuko pamoja na Qurani na Qurani iko pamoja na Ali, hawatoachana (tengana) mpaka watakaponijia huko hodhini (mwa kauthar), nami niwaulizeni mlicho watendea baada yangu”.([9])

Na kuna mfano wa hadithi hii katika Addaru Qutni.([10])

Ibnu Hajar, baada ya kuwa tumenakili kutoka kwake ya kwamba hadithi hii imepokewa kwa njia nyingi za wapokezi amesema kuwa “(Tuna-pata kwamba) katika, baadhi ya njia hizo za upokezi, Mtume Mtukufu (s.a.w.a) aliyasema (maneno haya) akiwa Arafa na katika njia nyengine (tunapata kuwa) alisema akiwa Ghadir Khum, na katika njia nyengine alisema akiwa Madina katika ugonjwa wake, na huku chumba kimejaa maswahaba wake, na katika njia nyingine alisema aliposimama kuhotubia baada ya kutoka (mji wa) Taif, wala hakuna kupingana kwa maneno, kwani hakuna ubaya wowote katika kukariri katika sehemu hizo na nyinginezo ili kuonyesha umuhimu wa Kitabu Kutukufu na kizazi chake kitoharifu” ([11]).

Bila Shaka, Ibnu Hajar ametoa faida njema na kutenda wema kwa maneno aliyoyasema, kwani kuka-riri hakukuwa ila tu kwa ajili ya umuhimu uliomo katika mambo haya ili asibaki yeyote na udhuru katika hayo kama alivyoseme Mtume (s.a.w.a) katika kauli yake:

((وقد قدمت اليكم القول معذرة اليكم))

“Nami nimewatangulizieni kauli hii ili msiwe na udhuru (wa kutoa baada yake)”.

Arafa, Mina, Ghadir Khum, hotuba ya mwisho, na katika hali ya ugonjwa aliofariki nao, ni mfano wa sehemu na nyakati ambazo kiongozi hawezi kuzungu-mzia ila tu yale yenye uhusiano kamili na uhai na mustakbali wa uislamu na waislamu.

Kwa hivyo kukariri kulikotajwa, na hususan katika sehemu na nyakati zilizotajwa, pamoja na joto kali na msongamano wa watu na hasa katika siku ya mwisho wa uhai wake na katika ugonjwa aliofariki nao; kisha kuwajulisha waislamu kuhusu kifo chake, kulikuwa na lengo la kuwaelekeza waislamu kwenye jambo hili muhimu. Basi ni juu yetu na ndugu zetu waislamu (Mwenyezi Mungu awazidishie utukufu na sharafa) kufikiria kikamilifu kuhusiana na yaliyoelezwa katika hadithi hii tukufu, kisha kutenda kufwatana na maagizo yali yomo ndani yake..

Na yatupasa kujua pia, je sisi ni katika washikama-nao na Qurani na kizazi cha Mtume Mtukufu (s.a.w.a) au la?

Naapa kwa uhai wangu kuwa hii hadithi tukufu inayokubaliwa na waislamu wote, inatosha kuwa-bainishia waislamu njia sahihi na kuwasahilishia njia za kupata umoja na maafikiano baina yao.

Ewe ndugu muislamu, fikiria, taamuli na kuitakasa nafsi yako, kwani njia iko wazi, wala usiyakhalifu aliyousia Mtume Mtukufu (s.a.w.a) katika hali tofauti tofauti na katika hali zenye uzito na umuhimu mkubwa.

Basi wajibu wetu mbele ya maneno ya Mtume (s.a.w.a) ni kuyafikiria kisha kutenda kufwatana nayo, na kisha kuyaeneza katika pembezoni mwa ardhi ili kuiga mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.a) kama alivyofanya Abu dhar (r.a) alipoishika sehemu ya mlango wa kaaba na kusema mbele ya watu (walio-kuwepo) “Mimi nilimsika Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema”:

((إني تارك فيكم الثقلين: كتاب الله وعترتي فانهما لن يفترقا حتى يردا عليّ الحوض فانظروا كيف تخلفوني فيهما)).

“Hakika mimi ninaacha kati yenu vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, kwani havitatengana kamwe mpaka vitakaponijia katika hodhi (ya kauthar). Basi angalieni mtakavyovitendea baada yangu”.([12])

 

Kusimamisha hoja kwa kutumia hadithi hii

Amirul Muuminin Ali (a.s) alitoa hoja kwa kutumia hadithuth thaqalain katika kikao cha shura ili kuthibitisha haki aliyokuwa nayo ya kuwa khalifa zaidi ya yeyote mwingine.

Ibnu Almaghazili amenakili kwa isnadi yake (njia ya upokezi) kutoka kwa Aamir ibnu waathila aliyese-ma “Nilikuwa chumbani pamoja na Ali siku ya shura nikamsikia akiwaambia (waliokuwemo);

((لأحتجنَّ عليكم مما لا يستطيع عربيكم ولا عجميكم بغير ذلك)) ثم قال: ((انشدكم بالله ايها النفر جميعاً أفيكم احد وحّد الله قبلي؟)) قالوا اللّهم لا ـ الى ان قال ـ ((فانشدكم بالله اتعلمون ان رسول الله (ص) قال: اني تارك فيكم الثقلين: كتاب الله وعترتي لن تضلوا ما استمسكتم بهما ولن يفترقا حتى يردا علي الحوض؟)) قالوا: اللهم نعم))

“Ninawahakikishieni kuwa nitawatolea hoja (yangu) kwa kitu ambacho hawezi mwarabu kati yenu na wala muajeni kati yenu kutoa hoja zaidi yake”, kisha akase-ma “Nawaapizeni (nyote) kwa (Jina la) Mwenyezi Mungu, enyi kikundi (cha waliopo hadharani) Je, kuna yeyote kati yenu aliyempwekesha Mwenyezi Mungu kabla yangu?” Wakajibu “Twaapa kwa (Jina la) Mwenyezi Mungu ya  kwamba hakuna (yeyote kati yetu)” mpaka akafikia kusema “Basi nawaapizeni kwa (Jina la) Mwenyezi Mungu, je mnajua ya kwamba Mtume Mtukufu (s.a.w.a) alisemu kwambu, “Hakika mimi ninaacha kati yenu viwili vizito; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, hamtapotea kamwe mkidumu kushikamana navyo, na kamwe havitoachana mpaka vitakaponijia hodhini (mwa kauthar)?” wakajibu “Twaapa kwa (Jina la) Mwenyezi Mungu kuwa ndio (tulimsikia akisema vivyo)”.([13])

Vile Vile Amirul Muuminin (a.s) alitoa hoja kwa kutumia hadithi hii katika Msikiti wa Mtume (s.a.w.a) katita ukhalifa wa Uthman mbele ya kikundi cha maswahaba, nao wakamjibu kwa kusema.

((نشهد ان رسول الله (ص) قال ذلك))

“Tunashuhudia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema hivyo”.([14])

Vile Vile Imam Hasan bin Ali (a.s) alitoa hoja kwa kutumia hadhithi hii ili kuthibitisha kuwa yeye ndiye aliyekuwa na haki ya kuwa khalifa na Imamu wa waislamu. Sheikh Suleiman Alqanduzi katika Kitabu cha Yanabiul Mawadda amenukuu kutoka kwenye Kitabu kiitwacho Almanaqib, hadithi kutoka kwa Hisham ibnu Hassaan, ya kwamba alisema.

((خطب الحسن بن علي(ع) بعد بيعة الناس له بالامر فقال ((نحن حزب الله الغالبون ونحن عترة رسوله الاقربون ونحن اهل بيته الطيبون ونحن احد الثقلين اللذين خلّفهما جدّي (ص) في امته ونحن ثاني كتاب الله فيه تفصيل كل شيء لا يأتيه الباطل من بين يديه ولا من خلفه)).

“Hasan ibnu Ali (a.s) alihotubia watu baada ya wao kumkubali kuwa khalifa na kusema, “sisi ndio kundi la Mwenyezi Mungu lenye ushindi, sisi ndio kizazi cha karibu cha Mtume wake sisi ndio Ahlubait wake walio wema. Sisi ndio kizito kimoja katika vizito viwizi alivyo viacha babu yangu (mpendwa) (s.a.w.a) katika umma wake. Na sisi ndio wa pili baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, (ambamo) ndani yake kuna upambanuzi wa mambo yote, haikifikii batili, mbele yake wala nyuma yake”.


 

([1]) Sunanut Tirmidhi J;5 uk; 662, H; 3786.

([2]) Mustadrakul Haakim. J: 3, uk: 109.

([3]) Sahihu Muslim, J: 4, uk: 187, H: 2408.

([4])Almu’ujamul kabir, J; 5, uk: 166, H: 4969.

([5]) Ihqaqul haqq. J:9, uk: 355.

([6]) Yanabiul mewadda J:1, uk: 116, chapa ya Islambul.

([7])Ghaibatun Nu’umani uk: 43.

([8]) Arjahul Matalib uk: 341 chapa ya Lahor.

([9]) Yanabiul Mawaddah J: 1, uk: 38.

([10]) Wasilatul Ma’ad (iliyoandikwa kwa khati ya mkono) kama ilivyonakiliwa katika nafahatul Azhar J: 1, uk: 341.

([11]) Hadithuth Thaqalain cha Sheikh Qiwamud din Al-washnawi uk: 13 – 14.

([12]) Yanabiul Mawadddah J: 1, uk: 37.

([13]) Almanaqib cha ibnu Almaghazili uk: 112 – 155.

([14]) Yanabiul Mawadda j: 1 uk; 114 – 116.

 

index