back page

SAFARI YA IMAMU RIDHAA KUELEKEA MARW.

next page

 

Baada ya kufariki Imam Kaadhim (a.s) wadhifa wa kuuongoza umma ulichukuliwa na mwane Imam Ridha (a.s), ambaye umri wake ulikuwa ni miaka thelathini na mitano mbali na wadhifa wake aliopewa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) wa kuongoza umma alikuwa ni mhusiwa wa pekee wa baba yake mpenzi katika kuwaangalia ndugu zake wa kike na kiume, na wadhifa wake aliutekeleza bila ya wasiwasi, ingawa utawala wa Haroun ulijaribu mumwekea vikwazo kwa njia ya siri kwani hali haikumruhusu kudhihirisha uadui wake.

Katika mwaka wa 193 H, Haroun aliugua na kufariki dunia  na hivyo nafasi yake ilichukuliwa na  na mwanae Amin  lakini uongozi wake haukudumu zaidi ya miaka minne  kutokana na ugomvi baina yake na ndugu yake  aitwae  Maamun.

Maamun alikuwa ni ndugu yake Amin lakini alikuwa ni mtoto wa mama wa kifursi tofauti na Amin ambaye baba na mama yake walikuwa ni waarabu.

Mzozo uliokuwepo katika serikali ya  wana wa Abbasiya  katika kipindi hicho uliwayima kabisa fursa ya kuweza kumbughudhi Imam na wafuasi wake. Hivyo basi Imam alitumia fursa hii kwa kuwapa wafuasi wake malezi  na mafunzo halisi ya uislamu.

Baada ya Maamun kuchukua utawala alianza kazi ya  kujenga nguzo za serikali yake, lakini kwa kutumia hila na ujanja na miongoni mwa hila alizokuwa nazo ni kuwakusanya maulamaa na kutengeneza vikao vya kielimu ili kuwadhihirishia watu kwamba yeye ni mtu mwenye hekima, mjuzi na mpenda elimu na maulamaa, na kwa upande mwingine ili kutafuta kuungwa mkono na waumini, na alidhihirisha mapenzi ya uongo kwa Amirul muuminiina (a.s) na kumlaani Muawia.

Na pia kutokana na kuongezeka kwa nchi za Kiislamu na kuwepo wapinzani pembezoni mwao kulimfanya Maamun ajipendekeze kwa waumini ili wasiungane na wapinzani wake na kumwongezea matatizo. Hivyo basi alimteua Imam Ridha (a.s) kushikilia uongozi lakini kwa masharti. Kwa lengo la kuwahadaa  alawiyuun wana wa amirul-muuminina (a.s) na wafuasi wa Imam (a.s)  na lau Imam angelikubali uongozi huu hakuna shaka kwamba mashia wangeliwacha kuipinga serikali hii kwa kuwa Imam wao ni miongoni mwa viongozi katika serikali hiyo. Hivyo basi Maamun alijitahidi awezavyo ili afikie lengo lake hili.

Alianza kwa kumwandikia Imam (a.s) barua za kumuomba akubali mwito wake huu. Lakini Imam (a.s) kujua lengo lake alimjibu waziwazi kuwa hayuko tayari kushirikiana naye katika jambo hili.

Maamun alipoona kwamba kwa upande wa barua hakuna dalili za  mafanikio aliamua kumtuma Rajai ibn Abi Dhahakar kwa Imam (a.s) ili amshawishi na aje naye katika mji wa Marw uliokuwa makao makuu ya serikali yake. Rajai alipomwendea Imam na baada ya kumalazimisha Imam (a.s) alilazimika kutoka katika mji wa Madina lakini kabla Imam hajaondoka katika, aliamua kufanya ziara  katika kaburi la babu yake Mtume (s.a.w) na maimamu na wengine katika makaburi ya Baqi, Kisha aliwaaga wanae na nduguze wa kike na kiume akiwemo miongoni mwao dadake mpendwa Sayyida Fatimah Maasumah (a.s). Haya yalifanyika katika mwaka wa 200 H.

Kisha sasa ukaja ule wakati mgumu sana katika maisha ya kila yule ambaye anaagana na vipenzi vyake na hasa familia yake.  hali hiyo ilimkuta Imamu pia kabla ya kuondoka, baada ya kukamilisha ziara zake katika haramu zote tukufu, alikwenda kuiaga familia yake na watu wake wa karibu watoto wake watoto wa ndugu zake na dada zake akiwemo Fatuma maasumah dada yake kipenzi na kisha akajiandaa kuondoka kuelekea Marw.

Yalikuwa ni majonzi huzuni na masikitiko makubwa katika familia ya Imamu pindi alipokuwa akiagwa na kuwaaga ndugu na jamaa zake wa karibu.

 

Na sii wao peke yao waliokuwa na huzuni kiasi kile bali hata na Imamu pia alikuwa katika hali ngumu sana kuvumilia na kuonyesha utulivu katika hali ya kuwaaga wapendwa wake na kwa kuwa pia watu wengi sana walikuwa wakimpenda sana Imamu kitu kilichosababisha majonzi makubwa baina yao na walikuwa ndio kimbilio lao pindi wanapokuwa na matatizo yoyote yale.

Na katika kufunga kwake safari Imamu Ridhaa ulionekana kama ndio mwisho wake wa kumsaidia dada yake mpenzi bibi Faatma ambaye baada ya kile kifo cha baba yake alionekana kumtegemea zaidi kaka yake mpenzi Imamu Ridhaa, kwa hiyo kule tuu kuondoka kwa Imamu halikuwa tu ni pigo na majonzi kwa wale watu wanaompenda Imamu, bali na hata ndugu zake na mwenyewe Imamu Ridhaa na hasa bibi Faatuma.

Baada ya kukubali kwake Maamun alifurahi sana lakini alifanya mikakati ya hali ya juu kuhakikisha ya kwamba msafara wa Imamu haupitii katika mapito au miji ambayo ilikuwa inasadikika ya kwamba ndio iliyokuwa na mashia wengi na akikhofia ya kwamba iwapo angepita katika maeneno hayo lazima kungetokea mapinduzi makubwa dhidi yake kwa hiyo aliona kwa namna ambayo watu walikuwa na mapenzi na Imamu laiti kama akiruhusu basi serikali yake inaweza kuangushwa hata kabla ya malengo yake na katika historia tunakumbushwa ya kwamba katika miji ambamo wakazi wake wengi walikuwa na mapenzi mazito na Imamu na Ahlulbayti wa Mtume wetu mtukufu rehema na amani za mwenyezi Mungu ziwe juu yake na ahli zake pia ilikuwa ni miji ya Kuufe, na katika mji wa Qom, jambo hilo halikuwa  na chembe ya wasiwasi wala shaka juu yake kwani lilikuwa lii wazi, Na hivyo safari yake ilifanyika bila hata kupitia miji hiyo.

Lilijitokeza jopo la wapenzi wa Imamu katika kila mji aliopita akielekea Marw japokuwa miji hiyo haikuwa ni miji ya mashia, lakini waumini walijitokeza kwa wingi ili kumlaki na pia walimpokea mapokezi ya pekee na ya aina yake na wengi sana walifurahia Imamu kuingia katika miji yao kwani walikuwa na shauku ya kuchota elimu kutoka katika mji na kiini chake.

Hata miji mingine ya Iran katika mapito ya Imamu walimpokea kwa kila aina ya shamra shamra nderemo na vifijo na kwa furaha zisizo na kiafani wala mfano katika historia.

Walikuwa wanafurika wanamji na kukizunguka kipando cha Imamu huku wakifaidika na kuwepo kwake katika mji ule, Naisaburi ni moja katika hiyo miji ambayo wakazi wa miji walipata khabari za kuwepo na kuja kwa mjukuu wa Mtume wetu mtukufu rehama na amani za mwenyezi Mungu ziwe juu yake na jamaa zake pia, walitoka majumbani mwao kwa shangwe huku wakienda na msafara na wakifaidika na maneno ya Imamu, walikuwa wakiichuma elimu kutoka katika shina lake, huku wakisema “Ewe mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu tunapenda kuchukua elimu kutoka kwako na pia  tusikie maneno mazuri kutoka kwako”.

Imamu aliwakubalia na kisha akawasomea hadithi ambayo silsila yake ni sahihi kutoka kwa baba yake ambaye naye ameipokea toka kwa Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu kuwa anasema,

“hakika amesema Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na aliyetukuka ya kwamba,neno“LAA-ILAHA-ILLA-AllAHU”Yaani hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki zaidi ya Mwenyezi Mungu  mmoja peke yake” hii kalima ni ngome na atakaye ingia katika hii ngome ameepukana na adhabu kali siku ya kiama, alipokwisha kusema hayo alikipanda kipando chake na  na baada ya kutembea hatua  chache akageuka na kuwaambia watu lakini kwa masharti yake na mimi ni miongoni mwa masharti hayo.

Na alikuwa Imamu na anamaanisha kwamba neno “LAA-ILLAHA-ILLA-AllAH”pekee halitoshi kwa mtu kuingia peponi bali msemaji ni lazima awe anawamini maimamu na miongoni mwao ni Imam Ridhaa, na katu hakuna yeyote atakayeweza kuipata imani ya kweli bila ya kuwaamini Ahlulbayti wa Mtume wetu mtukufu Rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu  yake na ahly zake na hiyo ndiyo njia pekee ya kumjua Mwenyezi Mungu mmoja na wa pekee na   mwingi wa Rehema.

Baada ya safari ndefu ya kupita katika mjangwa na mabonde milima mirefu na tambarare, safari iliyowagharimu siku kadhaa njiani hatimaye sasa ilifika katika mji wa Marw katika himaya ya Maamun ambaye katu hakukubali uongozi wa mwingine yeyote zaidi yake mwenyewe, aliukataa hata uongozi wa ndugu yake mwenyewe wa baba mmoja, na hata kwa upande mwingine Imamu naye alikuwa thabiti katika msimamo wake na wala haikuwa ni rahisi kwake kuukubali uongozi wa Maamun.

Na hivyo basi kutoelewana kati yao kuhusiana na jambo hili kuliendelea kwa muda wa miezi miwili. Lakini mwishowe Imamu alilazimika kukubali kutokana na shinikizo la Maamun.

Na ilipofika siku ya tarehe 7 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani katika mwaka wa miambili na moja (201) baada ya hijira ilikuwa ni siku ngumu na nzito kwa Imamu pale alipolazimika kuukubali uongozi huo wa pamoja, yaani yeye na Maamuni washirikiane kuendesha uongozi kwa kile alichokikusudia Maamun ya kwamba Imamu angekuwa ni mrithi wake wa uongozi baada yake yeye, lakini japokuwa Imamu alikubaliana na Maamun lakini alitoa sharti kwamba yeye asingejiingiza wala kujihusisha kwa namna yoyote na uongozi huo na Maamun, na walikubalina na sharti hilo.