back page

MWANZO WA MATATIZO NA KIFO CHA IMAMU KAADHIM (A.S).

next page

 

Viongozi katika zama hizo walikuwa wakiwaudhi sana watoto na wajukuu wa Mtume wetu Mtukufu (s.a.w) na haswa Imamu Kaadhim (a.s) katika zama hizo Imamu Kaadhim alikumbwa na matatizo, misukosuko, vitimbi vya kila aina pamoja na ujeuri aliofanyiwa na viongozi hao. Udhalimu ambao ulimsababishia matatizo mengi, Matatizo hayo alioyokuwa akiyapata Imamu Kaadhim (a.s) yalijaza majonzi katika moyo wa bintiye mpenzi bibi Fatima Maasumah, na mtu pekee aliyekuwa akiituliza na kuitunza familia ni kaka yake mpenzi Imam Ridhaa (a.s).

Katika zama hizo Imam alikutana na wafalme watano kutoka katika kizazi cha “Abass”, nao ni kama vile:-

(1)    Abu al Abbas al Safah,

(2)    Mansour al Dawaniq,

(3)    Na Hadi.

(4)    Na Almahdy

(5)    Na Haroun.

Na kila mmoja katika watawala hawa madhalimu walimuonjesha Imam (a.s) na kizazi kilichotokana na Imamu Ali (a.s) vitimbi vizito na vyakutisha na waliwapa kila aina ya bughudha na mateso.

Pindi alipozaliwa Fatima Maasumah kilikuwa kimepita kipindi cha muda wa miaka mitatu tangu Haaroun Al Abassy wachukue uongozi. Kiongozi ambaye alikuwa na kila aina ya nishani na utukufu katika uwanja wa dhuluma na alikithirisha kukopoa na kudhulumu mali za waislamu, na alifuata zaidi matamanio ya nafsi yake na alijifakharisha na dunia hii.

Pamoja na mateso yote aliyopata, Imamu Kaadhim (a.s) katu hakupitisha hata sekunde moja kunyamazia ama kuvumilia ama kufumbia macho udhalimu wa wazi wa Haroun na khiana alizozifanyia uislamu na umma wa kiislamu kwa ujumla.

Kutokana na kauli ya mbora wa viumbe na kipenzi cha waja wema na wacha Mungu mtume wetu mtukufu (s.a.w) anasema hivi:- ((“Pindi itakapodhihiri bidaa (uzushi) basi na wajibu wa wale walio wajuzi na wasomi wadhihirishe elimu zao (katika kukemea jambo hilo la uzushi lililozushwa) na ikiwa hawakufanya hivyo basi laana ya mwenyezi mungu ii juu yao”.))

Imamu Kaadhim (a.s) alikuwa ni mkali na asiye na mzaha katika kuitetea haki kukataza mabaya na kuamrisha mema bila ya kumjali mtendaji wa kosa hilo ni nani na ana cheo gani, ni mfalme au kijakazi ni mtumwa au mngwana, kwa ajili hiyo Imam alisimama kidete kuponda na kupinga vikali siasa zisizo kuwa na mantiki za Haroun aliyekuwa akiiteketeza dini ya mwenyezi Mungu.

Na kutokana na kujua wazi msimamo wa kizazi kilichotokana na Imamu Ally (a.s) na hasa Imamu Kaadhimu (a.s) aliyekuwa amesimama kidete kupingana na uongozi wa kidhalimu uliokuwepo madarakani, Haroun alifanya kila njia kuhakikisha ya kwamba anawanyima sauti na haki zote wakitumia mali nyingi sana za waislamu katika kampeni zao hizo haramu kwa kuwapa wale wajuzi wa kutunga mashairi ili wawachafue.

Vilevile alikuwa akiwafunga waumini katika njia ya kuwanyamazisha na hasa wale waliotokana na kizazi cha Imamu Ali (a.s), au aliwafanyia kampeni na kuwatenga mbali na jamii, na kuwauwa wengine waliokuwa na msimamo thabiti baada ya mateso mengi sana gerezani. 

Baada ya kupata nguvu serikali yake ya kifidhuli na dhuluma katika miji ya kiislamu, aliamuru Imamu Kaadhimu (a.s) awekwe chini ya ulinzi mkali na kisha afungwe ili kupunguza upinzani aliokuwa akiupata toka kwa mchamungu huyo.

Bibi Fatuma alipozipata khabari hizi alijawa na huzuni huruma na majonzi juu ya mzazi wake huyu kutokana na faida nyingi na zisizoelezeka walizokuwa wakizipata kutoka kwake kwani alikuwa ni kiumbe asiyekurubiwa kwa utendaji wake wa mema katika zama hizo, na haya yalitokea katika kipindi cha mwisho cha maisha yake matukufu.

Na masikitiko yalizidi pale alipoona ya kwamba sasa atamkosa moja kwa moja baba na mlezi wake wa pekee.

Wakati haya yote yanatokea umri wa bibi Fatuma ulikuwa chini ya miaka kumi, kwa hiyo alipata machungu yasiyoelezeka kwani kutokana na umri wake mdogo alikuwa akimhitajia sana baba yake mzazi ambaye sasa walikuwa wanatengana naye, hivyo alilia sana kwa uchungu.

Hata kwa Imamu Kaadhimu pia ulikuwa ni mtihani mkubwa kwake kwa kutengana na kizazi chake haswa wanawe wema aliokuwa akiwapenda sana Imam Ridhaa na bibi maasumah (a.s) na hivyo kuwajibika kufanya subira ya muda mrefu baada ya kutengana na familia yake.

Kutokana na ibada nyingi na utajo wa Mola wake Imam Kaadhim aliweza kukibadilisha kiza cha gerezani na kuwa nuru, katika siku hizo ngumu.

Lakini moyo wake ulizidi majonzi kila alipomkumbuka familia yake na hasa mwanae Fatuma Maasumah ambae alitamani sana kuwa nae.

Katika miaka miwili ya mwisho ya maisha ya Imamu Kaadhimu, Haroun alikuwa amefanya kampeni ya kumhamisha Imamu toka gereza moja hadi jingine hadi alipompeleka kwenye gereza la Issa bn Jaafar lililokuwa Basraa na huko alikaa kwa muda wa mwaka mmoja.

Na haikuwa kazi ngumu kwa mtu kama Imamu Kaadhim kutokana na tabia yake njema kuwaathiri kiasi kikubwa walinzi wa magereza ambao waliishia kuuwawa kikatili na wakuu wao, na wengine waliamua kujiuzulu kabla ya kugundulika na wakubwa zao.

Imamu alizidi kuhamishwa kutoka gereza hadi jingine na baadae alihamishiwa kwenye gereza lingine katika mji wa Baghdad kwa amri ya Haroun. Imamu alifungwa katika magereza tofauti kama vile:-

(a)      Fadhili bin Rabii kisha    

(b)     Fadhili bin Issa na mwishoni alihukumiwa katika Gereza la

(c)     Sanady   bin Shaahik.

Na sababu ya kuhamishwa kwake kote huko ni kutokana pia na ile azma ya Haroun kutaka kumuua Imam (a.s) lakini walinzi wote wa magereza ambao ndio haswa waliopewa jukumu hilo la kutimiza udhalimu huo walishindwa kukubali kuitii amri ya bwana wao na kuidhulumu nafsi hiyo isiyoukuwa na hatia, na hii pia inatokana na kwamba walinzi wengi kutoka katika kila gereza alilokuwa akifungwa Imam waliathirika vibaya na tabia yake na hata nyoyo zao zikajawa na mapenzi naye na kuamua kumfuata.

Hali hiyo iliendelea hadi pale Sandy bin Shaahika alipoamua kumpa Imam sumu kwa kutekeleza amri aliyopewa na Haroun.

Baada ya kutendeka jambo hilo Haroun alijua ya kwamba kutokana na mapenzi mazito ambayo watu walikuwa nayo juu ya Imamu, kama tu wangelihisi ya kwamba yeye ndiye hasa aliyehusika na kifo chake kwa amri ya kwamba apewe sumu ndani ya gereza na amefia katika mikono yake, matokeo yake yangekuwa ni mabaya na ya khatari sana juu hake.

Kwa khofu hiyo alilazimika kufanya kila aina ya mbinu ili kuuficha ukweli huu mbele za watu waliokuwa na mapenzi mazito juu ya mjukuu huyo wa Mtume wetu mtukufu (s.a.w.a).

Alijikuta akifanya kila aina ya mbinu na hila na moja katika mbinu zake ilikuwa ni kuwakusanya watu makundi kwa makundi ya mashia katika mbinu za kuwapumbaza na kuwaficha na ukweli halisi na kuongozana nao hadi kwa Imamu ili yashuhudie ya kwamba Imamu alikuwa ni mgonjwa na wala kifo chake hakimshirikishi na wala hakikuhusiana naye kwa namna yoyote ile.

Lakini kutokana na uchaji, hekima na werevu wa Imamu aligundua wazi hila za Haroun. Hivyo alimfanya Haroun afedheheke na hila zake kwani baada ya Imamu kulibaini hilo aliliweka wazi mbele ya wapenzi wake waliokuwa wanamzuru ya kwamba anasumbuliwa na maradhi yaliyotokana na sumu kali aliyopewa na kuathiri mwili wake mtukufu kwa kusema, “Hakika mtu huyu amenipa punje tisa za tende zilizotiliwa sumu kali na dalili ya kuthibitisha hayo ni kuwa kesho mwili wangu utabadilika rangi kutokana na hii sumu niliyopewa na baada ya kesho ndipo nitakapoaga dunia.

Na ukweli wa maneno ya Imam ulidhihiri manamo tarehe ishirini na tano katika mwezi wa rajabu mnamo mwaka wa 183 H siku mbili tuu baada ya maneno yake (a.s), alifariki dunia akiwa ni shahidi kutokana na sumu kali aliyopewa na adui yake na ndiyo siku iliyotimu ile safari yake ndefu ya milele isiyo na mwisho na ni siku aliyokutana na maimamu wenzake waliotangulia, na baba na babu zake pia.

Pindi shia walipopata khabari za kifo cha Imamu Kaadhimu (a.s) walivaa mavazi ya huzuni wakiomboleza kwa majonzi mazito kwani walikuwa wamempoteza kiongozi na mtetezi wa haki waliokuwa wakimpenda sana kwa kila tendo lake na kwa hilo huzuni zao zilionekana waziwazi juu ya nyuso na nyoyo zao, na miongoni mwa waliojawa zaidi na huzuni ni pamoja na mtoto wake Imamu bibi maasuma ambaye alikuwa na umri mdogo sana wakati huo zilipotokea habari hizi za kutisha na za kuumiza za kufiwa na baba yake mpendwa ambaye alimsubiri kwa hamu kubwa kwa muda wote aliokuwa gerezani, akiwa  na matumaini ya kwamba huenda baba yake angerejea baada ya siku kadhaa, na hasa  alikuwa na matumaini na subira ya kwamba huenda baba yake mpenzi angetolewa gerezani siku iliyofuata, kwa hiyo siku zote alikuwa amejiandaa kumpokea baba yake  mpenzi kwa mapokezi ya hali ya juu angempokea kwa shangwe na furaha na kukaa  katika mabega yake matukufu huku akisikiliza maneno yaliyojaa hekima heshima na  mafunzo mema toka katika kinywa cha baba yake mpenzi.

Lakini kinyume chake alipokewa na khabari za kusononesha na kuumiza sana pale alipolazimika kuupokea mwili wa baba yake mpenzi ukiwa umelala usingizi usio na mwisho.

index