back page

SAFARI YA BIBI  MAASUMA  KUTOKA MADINA KWENDA MARW.

next page

Kilikuwa kimepita kipindi cha mwaka mmoja tangu Imamu Ridhaa (a.s) aondoke katika mji mtukufu wa Madina na kuelekea Marw, jambo hili liliwaathiri kwa kiasi kikubwa ndugu na jamaa zake waliokuwa katika mji wa Madina na hasa Ahlulbayti (a.s) waliokuwa wamebaki Madina. Wote walikuwa ni wanyonge kwa kukikosa kipenzi chao ambacho walikuwa bado wakizihisi hisia zake na zile neema alizokuwa nazo pindi walipokuwa karibu naye na ilikuwa ni vigumu kwa hisia ndoto na mapenzi waliyokuwa nayo juu ya Imamu kuwatoka haraka kiasi hichi na sasa walikuwa na hamu na shauku ya kutaka kuonana tena na Imamu (a.s).

Fatuma Maasuma (a.s) kama walivyokuwa kaka na dada zake yeye pia alijawa na huzuni na shauku ya kutaka kuonana na kaka yake, kwani kule kumkosa kwake Imamu kulizidi kumhuzunisha kila kulipokucha. Imamu pia huko alikokuwa alikuwa  akiwakumbuka sana familia yake na hasa dada yake mpenzi Faatuma (a.s), na katika hali hiyo ndipo Imamu alipoamua kuandika barua kwa ajili ya dada yake na kumpa mmoja kati ya wasaidizi wake kwenda katika mji mtukufu wa Madina kupeleka barua hiyo lakini kwa masharti ya kwamba asisimame njiani wala sehemu yeyote hadi afike katika  mji mtukufu wa Madina haraka iwezekanavyo. Hivyo kabla ya kuondoka huyo bwana, Imamu alimwelekeza hadi katika nyumba aliyokuwa akiishi baba yake na familia yake tukufu na alifanya hivi ili huyu bwana asije akamuuliza mtu mwengine yeyote kuhusu nyumba hiyo.

Kwa kutekeleza amri mjumbe aliyetumwa na Imamu Ridhaa (a.s) kupeleka barua alifika mapema katika mji wa Madina na kuukabithisha ujumbe aliotumwa mikononi mwa Fatuma maasumah. Japokuwa haikufahamika juu ya kiwango na uzito wa barua yenyewe lakini la muhimu tuu ni kwamba barua ile ilizidi kuamsha kuchochea na kutia hamasa ile nia ya kutaka kumuona ndugu yao, na kutokana na hali hiyo bibi maasumah hakusita kuwafahamisha ndugu zake kuhusu ujumbe ule na kwamba  alilazimika kuondoka Madina kwenda Marw kumfuata kaka yake na ndugu zake waliafiki na haraka wakaandaa mipango ya safari. ilipokamilika walianza safari ya kuelekea Marw msafara ambao uliwajumuisha bibi maasumah na ndugu zake wengine watano ambao walikuwa ni:-

(i)                Faadhil,

(ii)              Jaafar,

(iii)            Haady,

(iv)            Qaasim na Zaidi.

Pia bibi Maasumah na ndugu zake katika msafara huo waliongozana na watoto wa ndugu zake pamoja na watumishi wa kike na kiume. Safari ilianza na kila mmoja kichwani alikuwa akitafakari namna atakavyokutana na Imamu Ridhaa (a.s) Itakuwa ni furaha iliyoje kwao kukutana na kipenzi chao waliyetengana naye zaidi ya mwaka?

Hili ni suali ambalo kila mmoja laikuwa akijiuliza wakati msafara wa kuelekea Marw ulipokuwa unaanza harakati.

Msafara ulizidi kwenda kwa kasi huku wakipita milima na mabonde na kuhakikisha ya kwamba walikuwa hawasimami sehemu yoyote ile njiani isipokuwa katika mambo ya dharura tuu kama vile ibada na chakula, zaidi ya hayo hakuna jambo lingine ambalo liliweza kuwasimamisha njiani. Walizidi kutembea kwa kasi kadiri walivyoweza na huku wakizidi kupita miji na kuviacha nyuma yao vilima hivi na vile na hatimaye sasa msafara ulikuwa unaupa mgongo mji mtukufu wa Madina na kuzidi kuukaribia mji wa Marw.

Kwa kweli safari ya jangwani sii kama safari nyingine kwa hiyo haikuwa ni kazi rahisi kwa bibi maasumah na kundi lake kusafiri katika jangwa. Kwani ilikuwa ni safari ndefu na yakuchosha mno, hata baadhi ya nyakati ngamia zao zilikuwa zinalemewa kutoka na ugumu na uzito wa safari hiyo, lakini pamoja na hayo haikuwa hoja ya kuakhirisha safari au kufanya safari nzima ishindwe kuendelea, lakini kutokana na nuru, shauku, hamasa na mapenzi ya kukutana na kaka yao walijikuta wakipata mori na motisha uliowafanya wasahau taabu matatizo na uchovu wote wa safari hiyo ndefu na yenye matatizo mengi jangwani na kujilazimu kuendelea na safari.

Lakini safari ni safari kama zilivyo safari nyingine ndefu za jangwani ama sehemu nyengine yeyote kwani kila safari inakuwa na matatizo yake, na hata katika zama zile safari kama hizo

Zilikuwa pia na matatizo yake haswa za Jangwani kama hizi ambazo ziliulikuwa na khatari kubwa ya watekaji nyara ambao waliwavizia wasafiri na hata wafanyabiashara mbalimbali nje na mijini huko majangwani. Waliwavamia na kupora mali zao walizokuwa nazo vito vya thamani na hata vipando vyao. Na kuna nyakati zingine waliwauwa wale wamiliki wa mali hizo ili waweze kupata urahisi wa kuzipora mali hizo, na hili lilikuwa ni tatizo kubwa ambalo liliwakumba wasafiri wengi waliokuwa wakifnya safari ndefu jangwani, Hili lilikuwa ni tatizo lingine lililo msumbua sana bibi maasumah na ndugu zake katika msafara huo, lakini kutokana na shauku ya kuonana na kaka yao hilo halikuwa muhimu tena kwao kwani hasa baada ya kutawakul na kutaraji ulinzi kutoka kwa Mola wao walilisahau kabisa tatizo hilo wakiwa na wazo moja tuu lilokuwa likiwasumbua akili zao nalo ni kuonana na kaka yao mpenzi.

Hivyo safari iliendelea na siku baada ya siku walikuwa wakiikaribia sehemu waliyokuwa wameikusudia.

Zilipita sekunde, dakika, masaa, na hata masiku huku msafara ukizidi kusonga mbele na kuacha nyuma milima na mabonde na sasa hayakubaki masafa marefu kwa msafara kuingia katika ardhi ya Iran.

Lakini kutokana na matatizo na urefu wa safari bibi maasumah (a.s) alikuwa amechoka sana na hata ndugu zake wengine ambao alikuwa ameongozana nao katika safari hiyo. Lakini jambo lililokuwa likiwajasiri ni ile hamu na shauku ya kuonana na kaka yao mpenzi Imamu Ridhaa (a.s).

Marw ni moja ya mji katika nchi ya Iran kwa hiyo kila mmoja alikuwa akijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake wote ili angalao wakutane na kaka yao mpenzi Imamu Ridhaa, na walikuwa wakiyakumbuka masiku ambayo yalipita wakiwa pamoja katika mji mtukufu wa Madina, jambo hilo liliwapa matumaini mengi na kuwajaza furaha nyingi sana na hichi ndicho kitu kilichasababisha woga na uchovu ukose nafasi katika nafsi zao tukufu, na sasa kile kipindi kigumu cha shida na matizo ya safari ndefu yenye kutisha na kuchosha safari ya jangwani kilikuwa kimekwisha na sasa walikuwa wanaingia katika arthi ya Irani wakipita kijiji kimoja hadi kingine na mji mmoja hadi mwingine.

index