Ilikuwa ni tarehe 23 ya mwezi watatu (Rabiul Awal) mwaka wa 201 msafara wa bibi Maasumuah ulifika katika mji wa Qom na waliona fahari sana watu wa Qom na kutokana na ugeni huo uliowajia.
Na kwa upande mwingine bwana Mussa bin Khazraj alikuwa ni mtu mwenye nafasi nzuri kimaisha na alikuwa na nyumba ambayo ilikuwa na nafasi nzuri na ya kutosha na hivyo msafara ulipofika tuu Qom ulifikia moja kwa moja nyumbani kwake. Na kwa msafara wa bibi maasumah kufikia katika nyumba ya bwana Mussa ilikuwa ni furaha ya ajabu bahati na utukufu wa kipekee katika familia ya bwana Mussa na hata kwa yeyote yule ambaye angeweza kuipata fursa hiyo hivyo bwana Mussa alijikuta akiwa na furaha isiyosemeka kwa kupata nafasi ya kuwahudumia wageni wake waliotoka katika mji mtukufu wa Mtume wetu Mtukufu (s.a.w) mji wa Madina.
Na alijitahidi kuwahudumia kwa kadiri alivyoweza kwa kuwatayarishia kila jambo ambalo walilihitaji kwa haraka na uchangamfu wa hali ya juu.
Katika muda wote ambao bibi maasumah (a.s) alikuwa katika mji wa Qom alikuwa ni mwingi sana wa ibada na unyenyekevu akiomba kutoka kwa mola mwingi wa rehema na msamehevu aweze kumsahilishia yote aliyokuwa nayo na sehemu ambayo alikuwa akifanyia ibada bibi maasumah ipo hadi leo na huitwa “Nyumba yenye nuru”
Wakazi wa mji wa Qom pamoja na msafara mzima aliokuja nao bibi maasumah alikuwa na majonzi mazito kutokana na hali liyokuwa nayo bibi maasumah na japokuwa alikuwa ni mtumiaji wa dawa lakini bado hali yake ilizidi kuwa mbaya siku hadi siku na hii ilitokana na kwamba maradhi yake yalikuwa yameenea mwili wake wote.
Na siku ya kumi katika mwezi wa rabiu Thaani (Mwezi wa Kumi) mwaka wa mia mbili na moja 201 baada ya hijra mwezi wa kiarabu ilikuwa ni siku ambayo ilikuwa ni chungu kuliko siku nyingine zozote katika Ahlubayti walio ongozana na bibi maasumah katika msafara wao na watu wa Qom pia ni siku ambayo wapenzi wa Ahlulbayt walipata pigo lingine na pigo kubwa kuliko lile la mwanzoni. Pigo ambalo kwamwe sii la kusahaulika kwani liliandikwa katika vitabu vya historia ili kila mtu alielewe nayo ni siku hiyo ambayo bibi maasumah alifariki duni alifariki dunia bila hata ya kutimiza azma yake ya kutaka kukutana na kaka yake mpenzi Imamu Ridhaa ambaye yeye alikuwa katika mji wa Marw. Hata kabla ya kifo chake bibi maasumah alikuwa akibubujikwa na machozi na moyo wake kugubikwa na wimbi la huzuni kwa kutengana na kaka yake na hata alipoondoka katika mji mtukufu wa Madina kwa lengo moja tuu la kuja kumuona kaka yake mpenzi lakini sasa alikuwa anafariki dunia bila hata kumwona tena kwa mara ya mwisho kaka yake mpenzi, na wakati huo bibi maasumah alikuwa na umri wa miaka 28.
Walipigwa na butwaa watu wa Qom kutokana na msiba huo uliowapata na hawakuweza kabisa kuzuia huzuni zao zilizojaa nyoyoni mwao kwa kuondokewa na kipenzi chao, na hivyo basi waliweka vikao vya kuombaoleza msiba huo.